Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-
Viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislamu mkoani Tabora wamesisitiza umuhimu wa kulinda amani na mshikamano wa kitaifa, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu. Wamesema Watanzania wanapaswa kuendeleza tabia ya upendo na kusaidiana ili kujenga mfumo bora wa kiuchumi na kijamii.
Kauli hiyo imetolewa katika hafla ya uzinduzi na ufunguzi wa Msikiti mpya uliojengwa katika kijiji cha Chesa, Wilaya ya Uyuwi, mkoa wa Tabora, kupitia Taasisi ya TAIZA, ambayo inajihusisha na kusaidia watoto yatima, wajane na wazee.
Dkt. Miymari, mgeni rasmi wa hafla hiyo, alisisitiza jamii kujenga utamaduni wa kusaidia wenye uhitaji, akisema:
"Nawausia kufanya matendo mema ya kumcha Mwenyezi Mungu, kama vile kusaidiana ninyi kwa ninyi, na mkifanya hivyo mtakuwa mmemfurahisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad (s.a.w.w)."
Kwa upande wake, Dkt. Swaleh Maulid alieleza faida za msikiti katika jamii, akisema:
"Msikiti ndio unaotoa ramani ya kesho ya jamii, ni sehemu ya kuwaunganisha watu na kuboresha imani zao. Kwa ibara nyepesi, msikiti ni kituo cha malezi ya kiroho."
Aidha, alisisitiza juu ya umuhimu wa kujenga Misikiti kwa ajili ya ibada na malipo yake makubwa, akibainisha kuwa:
"Kujenga Msikiti ni miongoni mwa mambo ya haraka na ya msingi aliyoyafanya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w), na mara zote aliwasisitiza waumini kujenga Nyumba za Mwenyezi Mungu (swt)."
Kisha akamnukuu Mtume (s.a.w.w) akisema:
عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:
مَنْ بَنَى مَسْجِدًا لِلَّهِ تَعَالَى خَالِصًا لِوَجْهِهِ، ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِهِ سُبْحَانَهُ، بَنَى اللَّهُ لَهُ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ مِثْلَهُ، حَتَّى وَإِنْ كَانَ هَذَا الْبِنَاءُ شَيْئًا يَسِيرًا جِدًّا.
Imepokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w):
"Yeyote atakayejenga msikiti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa ikhlasi na kutafuta radhi Zake, basi Mwenyezi Mungu atamjengea nyumba Peponi mfano wake, hata kama huo ujenzi ni mdogo sana na wa thamani ndogo."
Your Comment